Wednesday, 4 June 2014

IDARA YA WATOTO ICC YAHITIMISHA KILELE CHA WIKI YA SIKUKUU YAO

Siku ya Jumapili tarehe 01/06/2014 Idara ya Watoto na Uanafunzi ya ICC imehitimisha rasmi kilele cha Wiki ya Sikukuu ya Idara iliyoanza wiki iliyopita. Katika kuadhimisha Sikukuu hii shughuli mbalimbali Kanisani zilisimamiwa na Idara hii inayojumuisha Watoto, Waalimu pamoja na Wafadhili wa Idara hii.

Ingawa kulikuwa na changamoto ya kutokuwa na umeme pia jenereta kupata hitilafu, lakini Sikukuu ilikuwa njema na ilipendeza sana. Ibada ya kusifu na kuabudu iliongozwa na Timu kwa kushirikiana na Watoto.


Ibada ilikuwa nzuri sana ambapo Watoto walionesha uwezo mkubwa katika mambo mengi sana. Idara iliwatia moyo Watoto waliofanya vizuri katika masomo yao Idarani, Watoto waliofanya vizuri walipewa zawadi mbalimbali.

Tukio lililovuta hisia za watu wengi ni kuhamishwa kwa Watoto kutoka Idara ya Watoto kwenda Idara ya CA's baada ya kukidhi vigezo na masharti. Watoto hao walikabidhiwa kwa Kiongozi wa CA's Mwl. Ezekiel Fungo na Mchungaji wa Idara ya Watoto na Uanafunzi Mrs. Roswita Kitine. Baada ya kukabidhiwa, Watoto hao walifanyiwa maombi na Watumishi wa Bwana wakiongozwa na Mchungaji Mlezi Raphael Kitine pamoja na Mchungaji wa Idara Roswita Kitine.




Upande wa Neno la Mungu alihubiri Katibu wa Idara ya Watoto Sehemu ya Iringa Mrs. Mahona. Alihubiri ujumbe "ITAMBUE NAFASI YAKO KATIKA KUMLEA MTOTO"


Katika somo hili alifundisha kuwa Mungu ndio mwanzilishi wa Familia, alipomuumba Adam na Hawa. Pia alifundisha kuwa Familia ndio mwanzo wa Kanisa, Familia zikiwa vizuri basi hata Kanisa pia litakuwa vizuri. Alisisitiza kuwa Wazazi wengi wanawarithisha Watoto miungu bila wao kujua, mfano biashara, kazi n.k Lakini Wazazi wana wajibu wa kurithisha Watoto wao Mungu wa Kweli.

Pia Wazazi wanapaswa kuambatana na Watoto wao kwenda Ibadani na si kuwaacha nyumbani, akatoa mfano wa Musa alipoulizwa na Farao anataka kuondoka na nini, Musa alijibu ni pamoja na Watoto wao (Kutoka 10:8-9); hivyo nasi hatupaswi kuwaacha Watoto nyuma. Alifundisha pia kuwa Mzazi unapokuwa bize na shughuli zako na kushindwa kumfundisha Mtoto maneno yua Mungu, shetani naye atakuwa bize kumfundisha Mtoto wako mambo mabaya.

Mwisho akahitimisha kuwa ni Wajibu wa kila Mzazi kumlea Mtoto katika njia impasayo, Mithali 22:1-10.
Maandiko mengineyo ya somo: Torati 11:18-19; 1 Sam 2:18-21, 3:8.

Baada ya Mahubiri ilifanyika harambee ya kuchangisha pesa kwa ajili ya kununua viti vya Idara ya Watoto. Mungu ni mwema, ahadi na pesa taslimu zilipatikana ambapo jumla ya viti 98 vitanunuliwa mara ahadi hizo zitakapokamilika.

Harambee ya kutunisha mfuko wa Idara iliendelea, ambapo keki ilinadiwa.


Mwisho kabisa, Watoto na Kanisa zima walipata chakula kwa pamoja kuonesha upendo na ushirikiano.



Kilichofuata, ni kurudi majumbani.


Naomba radhi kwa muonekano wa picha sio standard sana!
Ubarikiwe, Karibu sana ICC Sabasaba.

No comments:

Post a Comment